Ndege iliyobeba watu 81 wakiwemo wachezaji wa klabu moja ya soka ya Brazil imeanguka eneo la Medellin nchini Colombia.

Ndege hiyo ilikuwa safarini kutoka Bolivia na ilikuwa imewabeba wachezaji wa timu ya Chapecoense, ambao walikuwa wamepangiwa kucheza mechi ya fainali ya Copa Sudamericana, dhidi ya timu ya Medellin, Atletico Nacional.

Mechi ya awamu ya kwanza ya kombe hilo, la pili kwa umuhimu Amerika Kusini, ilikuwa imepangiwa kuchezwa Jumatano lakini sasa imesitishwa.

Timu hito inayotoka mji wa Chapeco, kusini mwa Brazil, ilipandishwa kucheza ligi ya daraja ya kwanza nchini Brazil mwaka 2014 na ilifika fainali ya kombe hilo la Sudamericana kwa kulaza San Lorenzo ya Argentina.

Taarifa zinasema ndege hiyo muundo wa British Aerospace 146 ambayo imekuwa ikitumiwa na shirika la ndege la Lamia la Bolivia ilikuwa na abiria 72 na wahudumu tisa.

Ndege hiyo imeanguka eneo la milimani nje kidogo mwa mji wa Medellin majira ya saa sita usiku saa za huko (saa mbili asubuhi Afrika Mashariki).

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa maafisa wa uwanja wa ndege, marubani walisema ndege hiyo ilikuwa imepata matatizo katika mfumo wake wa umeme.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *