Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene amesema kuwa ameagiza fedha zilizotolewa kwa kaya zisizokuwa na sifa katika mpango wa kunusuru Kaya maskini unaofanywa kwa uratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kurejeshwa.
Waziri huyo amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri kuwasimamisha kazi waratibu wote wa TASAF wilaya ili kufanya uchunguzi wa jinsi walivyojihusisha katika kuvuruga utekelezaji wa mpango wa kunusuru Kaya maskini kwa kuandikisha kaya zisizokuwa na sifa.
Aidha aliitaja mikoa ambayo inaongoza katika uchakachuaji wa fedha hizo kuwa ni Dar es Salaam ambayo ina kaya zisizo halali na zimenufaika na mpango huo 2,929, Kilimanjaro 1,484, Shinyanga 521 na Morogoro 793.
Mikoa mingine ni Arusha ambayo ina 446, Dodoma 482, na Mbeya 465. Alisema mikoa ambayo imejitahidi kufanya halali katika mpango huo ni Kagera, Rukwa, Singida, Lindi, Mara na Mtwara.
Waziri ametoa siku 14 kuanzia juzi kwa wakuu wa mikoa kufikisha taarifa ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya watendaji waliojihusisha na upotevu huo wa fedha.