Rais mstaafu wa awamu ya tatu ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Benjamini Mkapa, amewataka viongozi wa vyuo vikuu nchi nzima kukutana kwa lengo la kujadili gharama za uendeshaji wa vyuo hivyo nchini.

Ametoa kauli hiyo wakati wa mahafali ya saba ya chuo hicho na kufafanua jambo hilo lisipozungumzwa sasa linaweza kuwa tatizo kubwa siku za usoni.

Amesema nchi bado changa lakini kwa sababu uchumi wa nchi ni mchanga kwa maana hiyo bado ni nchi masikini, hivyo wanajitahidi kukuza uchumi kwa kasi lakini matarajio na idadi ya wanachuo na wanafunzi ni kubwa na inazidi kukua siku hadi siku.

Amesema kukua huko ni lazima kufanane na uwezeshaji wa vyuo vyote kutoa elimu na kama bajeti hazitoshelezi yatapatikana matokeo hafifu na ushindani katika jumuiya ya Afrika Mashariki, Afrika na dunia nzima na kwa wahitimu hapa nchini utakuwa mgumu sana.

Mkapa amesema amri na maagizo peke yake hayatatui tatizo ila viongozi wakikaa pamoja wanaweza kujadili mikakati ya kugharamia jambo ambalo linanza kuimarisha ubora wa elimu na umakini wa rasilimali watu wanaotokana na vyuo vikuu vya serikali.

Amesema chuo cha UDOM kutegemea uwekezaji wakati chenyewe kinawekezwa ni kujidanganya, hivyo wakiamua kufanya mkutano wanaweza kupata ufumbuzi katika vyuo hivyo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *