Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Shirika la Posta Tanzania imetangaza kufukuza wafanyakazi wote wa shirika hilo waliojihusisha na ubadhirifu wa Sh bilioni 13 kupitia wizi wa mafuta ya magari ambayo yamekuwa yakilipwa kwa magari ambayo ni mabovu.
Hatua hiyo imekuja baada ya bodi hiyo kufanya ziara Dar es Salaam kwenye maeneo yaliyoonesha kuwa mikataba yake ina mashaka, ili kujiridhisha na kuchukua hatua.
Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dk Haruni Kondo amesema wamebaini ubadhirifu uliofanywa kwa magari mabovu ambayo yapo gereji, lakini yamekuwa yakipewa mafuta kwa miezi 18 ambapo gharama ya mafuta hayo imefika Sh bilioni 13 mpaka sasa. Alisisitiza watumishi wachache wanaofanya vitendo vya namna hiyo wataondolewa ili kuleta ufanisi katika shirika hilo.
Ameongeza kuwa ubadhirifu mwingine waliougundua ni ule ambao unafanywa na madereva wa magari ya mizigo ambayo yanakuwa yamesheheni mizigo ya Sh milioni 10, lakini inapofikishwa sehemu husika wahusika wanadai mizigo hiyo ni ya Sh 500,000.
Dk Kondo amesema suala hilo limekuwa ni tatizo kwenye mali za shirika hilo, kwani hata pale bodi inapotaka taarifa kwa ajili ya kujiridhisha inapata usumbufu.