Agizo la Rais wa Jamhuri wa muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli la kuweka mashine za kisasa za kukagua mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam umetekelezwa banadarini hapo.

Mradi wa kuweka mashine hizo za kisasa za kukagua mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam ambazo zina uwezo wa kusoma na kupeleka taarifa na picha za mizigo mubashara kwenye mifumo ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Mamlaka ya Mapato (TRA) umekamilika.

Kukamilika kwa mradi huo kunatokana na maagizo aliyoyatoa Rais John Magufuli kuwa TPA na TRA zishirikiane kuendesha mashine za kukagua mizigo zinazotoa taarifa na picha mubashara, pamoja na kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha Serikali haipotezi mapato na kupitisha mizigo haramu.

Kuwepo kwa mashine hizo kutazisaidia TPA na TRA kubaini shehena zilizoko kwenye makasha yanayofikishwa bandarini hapo kupelekwa na kutoka nje ya nchi kama inawiana na nyaraka za mzigo huo; na hivyo kutozwa ushuru sahihi kwa mzigo stahiki. Lengo la kufunga mashine hizo ni kuongeza mapato kwa serikali.

Meneja wa Mradi huo, Zhang Sheng alisema jana kuwa mradi huo umekamilika na sasa wako katika hatua ya pili ya mafunzo na skana hiyo mpya inaweza kutumika muda wowote mara baada ya kukamilisha mafunzo.

Kwa mujibu wa Meneja huyo kutoka China, skana hiyo ina uwezo wa kusoma na kupeleka taarifa na picha za mizigo mubashara kwenye mifumo ya TPA na TRA kwa wakati mmoja bila kuchelewa. Kutokana na kukamilika kwa mradi huo, TRA na TPA zimeanza kuwapa mafunzo watumishi wao namna ya kutumia mashine hizo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *