Wanachama na viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) wa wilaya za Mkoa wa Morogoro wamemwomba Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kutoa azimio la kujiengua ndani ya ushirikiano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Hatua hiyo ya wanachama na viongozi hao imetokana na wao kubainika ukiukwaji wa malengo ya kuasisiwa kwa umoja huo na badala yake ulitumiwa na vyama shirikishi kukihujumu ambapo kuanzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na ule Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka 2015.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano wa ndani wa chama hicho uliowashirikisha baadhi ya wanachama na viongozi wa kamati za utendaji za wilaya za Kilosa, Mvomero, Morogoro Mjini na Vijijini kichama, walimtaka Profesa Lipumba kuiondoa CUF ndani ya Ukawa kutokana na madhara makubwa waliyoyapata.
Katibu wa Wazee wa CUF Wilaya ya Morogoro Mjini, Mohammed Chunga alisema kutokana na kutokuwepo makubaliano ya kisheria ya kuachiana majimbo na kata kutoka miongoni mwa washirika, kumekiathiri chama kutokana na maeneo yaliyoachiwa CUF kuwekewa pia wagombea wa Chadema, hatua hiyo ni pamoja na ngazi za udiwani.
Hivyo amesema sehemu ambapo mgombea wa CUF alikuwa akikubalika, pia Chadema iliweka mgombea wake na kusababisha kura kugawanyika kitendo kilichokinufaisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mgombea wao kushinda kwa tofauti chache za kura.
Na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya CUF Wilaya ya Morogoro Mjini, Pilly Bilali, Awadhi Komba na Katibu mstaafu wa wilaya hiyo, Haruna Msuku, kwa nyakati tofauti walisema hakuna mwanaCUF asiyetambua Ukawa umewadhoofisha kisiasa upande wa Tanzania Bara na kikinufaisha Chadema, hivyo kutaka ijiondoe mara moja.
Hata hivyo, wanachama na viongozi hao walimpongeza Profesa Lipumba kwa uamuzi wake kurudi kwenye wadhifa wake na kwamba wataendelea kumuunga mkono ili arudishe hadhi ya chama hicho baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka jana.