Vifaa vinavyotumika kuhakiki vyeti kwa watumishi wa umma pamoja na kuandikisha Vitambulisho vya Taifa, ikiwemo kamera zenye thamani ya Sh. milioni sita vimeibiwa na watu wasiojulikana katika jengo la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.

Kamera mbili na viegesho vyake (stand), vimebainika kupotea jana asubuhi wakati wa kujiandaa kuendelea na kazi ya kuhakiki vyeti na kuandikisha Vitambulisho vya Taifa.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humu, Nyabaganga Talaba, alithibitisha kupotea kwa kamera hizo za Nida.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga pia alilithibitishia Nipashe kupotea kwa kamera mbili na viegesha vyake vilivyokuwa vimehifadhiwa kwenye ofisi ya halmashauri yake kwa ajili ya kupigia picha za Vitambulisho vya Taifa.

Hata hivyo, Magoiga amesema bado hajawapata undani zaidi kuhusu upotevu wa vifaa hivyo na watatoa taarifa kamili baadaye.

Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Muliro Jumanne Muliro, naye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo la upotevu wa vifaa hivyo na kusema kuwa uchunguzi unaendelea.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *