Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) linatarajia kufanya marekebisho ya kanuni ya michuano ya ligi ya mabingwa barani humo kwa kupendekeza ushiriki wa moja kwa moja kwa klabu ambazo zitamaliza kwenye nafasi nne za juu.
Mabadiliko hayo yatazihusu nchi za Uingereza, Italia, Uhispania na Ujerumani kutokana na kuwa na ligi bora.
Kamati ya mashindano ya UEFA imepenedeza kanuni hiyo ili iweze kufanyiwa mabadiliko katika mkutano mkuu wa wajumbe wa shirikisho hilo.
Kamati hiyo imesisitiza kupendekeza ili iweze kufanya kazi kati ya mwaka 2018-2021 kwa majaribio kuona kama itakuwa na mashiko yanayokusudiwa .
Kamati hiyo imependekeza kufanya marekebisho hayo baada ya kufanya uchunguzi na kubaini klabu ambazo zimekuwa zikimaliza katika nafasi ya nne zimekuwa zikishindwa kuitumia vyema nafasi hiyo baada ya kutolewa kwenye hatua ya mchujo ya mashindano ya klabu bingwa Ulaya.
Mapendekezo hayo yanatarajiwa kuwasilishwa katika mkutano mkuu wa UEFA utakaofanyika Septemba 14 na 15 nchini Uswizi.