Uongozi wa juu wa chama cha ZANU-PF umepuuza maneno ya mwanasiasa kijana wa Adrika Kusini Julius Malema aliloyatoa kupitia mtandao wa Facebook kwa kusema anashukuru kwa msaaa mkubwa ambao ‘Babu Mugabe’ ameutoa kwa Afrika lakini anaamini ni muda wa kiongozi huyo kung’atuka.
Kwenye taarifa yake, ilyotumwa na Psychology Maziwisa kwa njia ya mtandao huo huo wa Facebook, ZANU-PF imesema kuwa Julius Malema ni ‘mtoto na hahusiki’ na masuala ya Zimbabwe.
‘Hatushughulishwi na kauli ya sasa ya Julius Malema. Yeye ni mtoto na ni mtu asiyehusika ambaye anajaribu kila njia kupata umaarufu wa kisiasa nchini Afrika Kusini kwa kumtukana mtu mkubwa nchini Zimbabwe. Hawezi kushinda’.
Malema ambaye ni kiongozi wa chama kipya cha siasa nchini Afrika Kusini cha Economic Freedom Fighters (EFF) alichokianzisha baada ya kufukuzwa ANC, aliandika kwenye mtandao wa Facebook kuwa anaunga mkono jitihada za kuhakikisha utawala wa watu wachache nchini Zimbabwe unaondolewa lakini anaamini rais Mugabe anapaswa kujiuzuru.
‘Tunasema hili kwa upendo. Si kwasababu tunamchukia. Tunamsherehekea Mugabe, tunasherehekea kile alichokifanya na tutaendeleza urithi wa mtazamo wake, lakini babu anapaswa kujiuzuru sasa’.
Rais Mugabe ameshapitishwa na chama chake kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika mwakani licha ya kuwa atafikisha miaka 94 utakapofika wakati wa uchaguzi huo.